Mututho ataka Bunge lipitishe mswada wa kukabiliana na mihadarati

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya kitaifa ya kukabiliana na uraibu wa pombe na utumiaji mihadarati, NACADA, John Mututho ametoa wito kwa Bunge liharakishe kupitisha mswada wa kukabiliana na utumiaji mihadarati.

Amesema kuwa mswada huo utasaidia kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya nchini na kukabiliana na walanguzi na watumiaji sugu wa mihadarati kote nchini ambao husababisha maelfu ya vifo na kusambaratika kwa familia kila mwaka.

Mututho amesema hayo katika Kijiji cha Muchorwe, Eneo Bunge la Molo, wakati wa ibada ya mazishi ya Joana Koech, wa umri wa miaka 50 aliyeaga dunia baada ya kushambuliwa na waraibu wa mihadarati.

Marehemu Mzee Koech ameripotiwa kudhulumiwa na kulawitiwa kabla ya kuuawa nje ya kibanda kimoja cha utayarishaji pombe haramu kijijini humo.

Mututho aliwahimiza wabunge watafakari kuupa mswada huo umuhimu zaidi ili kunusuru maisha ya vijana.

Mswada huo unapendekeza kwamba walanguzi na watumiaji wa pombe haramu na mihadarati watozwe faini ya kati ya shilingi milioni tano na milioni 10 kama hatua ya kukomesha uovu huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *