Categories
Michezo

Musa Otieno ana imani ya Kenya kufuzu AFCON 2022

Aliyekuwa nahodha wa muda mrefu zaidi wa Harambee Stars Musa Otieno ana imani kuwa timu hiyo itashinda mechi mbili za kufuzu za mwezi ujao na kujikatia tiketi kwa kipute cha AFCON mwaka ujao nchini Cameroon.

Otieno ambaye ni mmoja wa washauri wa kiufundi wa FKF amesema ana imani na mbinu za ukufunzi za kocha Jacob Ghost Mulee baada ya kuiongoza timu hiyo katika makala ya mwaka 2004 nchini Tunisia akiwa nahodha.

“Katika soka kila kitu kinawezekana,nina imani na kocha Mulee,cha mhimu ni kujiamini na kupata matokeo katika mechi dhidi ya Misri hapa Nairobi na pia tushinde Togo ugenini “akasema Otieno

Kenya ni ya tatu katika G la kufuzu kwa pointi 3 wakati Comoros na Misri zikiaongoza kwa alama 8 kila moja na ili kujikatia tiketi kwenda Afcon kwa mara ya pili mtawalia Harambee Stars hawana budi kushinda mechi zote mbili zilizosalia dhidi ya Misri Machi 22 mwaka huu uwanjani Kasarani ,na kuilaza Togo tarehe 30 mwezi ujao na kutarajia kuwa Misri na Togo hawatazoa hata pointi moja katika mechi zao mbili zilizosalia.

Otieno amelitaka shirikisho la FKF kuweka mikakati ifaayo kuanzia kwa mashindano ya shule za sekondari kuhakikisha kuwa Harambee Stars inafuzu kwa fainali za kombe la dunia mwaka ujao nchini Qatar.

“majirani zetu wametilia maanani mashindano ya shule za sekondari na pia FKF inapaswa kuyazingatia mashindano hayo na tutengeze timu thabiti za chipukizi,cha mhimu pia ni benchi ya ukufunzi kuhakikisha Kenya inashinda mechi zote za nyumbani na kutafuta sare kadhaa ugenini au hata ushindi ili kufuzu”akaongeza Otieno

Kenya imejumuishwa kundi E la kufuzu kwenda Qatar pamoja na miamba Mali,Uganda na Rwanda huku mechi hizo zikianza mweiz Juni mwaka huu ambapo timu bora kutoka kundi hilo itatinga hatua ya mwondoano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *