Munyes: Serikali ya kaunti ya Turkana inahujumu ujenzi wa bomba la mafuta

Waziri wa mafuta na madini John Munyes amedai kwamba wanasiasa na serikali ya kaunti ya Turkana wanahujumu ujenzi wa bomba la mafuta kutoka kaunti ya Turkana hadi bandari ya Lamu.

Munyes alielezea wasiwasi wake kwamba viongozi kutoka kaunti ya Turkana wanapinga mradi huo huku kaunti nyingine nne zikiuunga mkono.

“Baadhi ya viongozi wapinga mradi huu. Ni jambo la kushangaza kaunti nne zinaunga mkono mradi huu lakini ni kaunti moja pekee inayopinga. Tatizo ni serikali ya kaunti ya Turkana ikizingatiwa kwamba inapaswa kuisaidia serikali kuu kufanikisha mradi huu,” alisema Munyes.

Alisema kaunti ya Turkana itanufaika zaidi na mradi huo ukikamilika. Aidha waziri huyo alifafanua kwamba suala la fidia litashughulikiwa na tume ya kitaifa ya ardhi kwa mujibu wa sheria kwani ardhi ya ujenzi wa bomba hilo hununuliwa sawia na ile ya ujenzi wa barabara na reli.

Aliongeza kwamba mradi huo hautaingilia ardhi ya kulisha mifugo kwa wafugaji.

Alitoa wito kwa viongozi waunge mkono mradi huo utakaowezesha kaunti hiyo kupata maji kutoka bwawa la Turkwel na hivyo kupiga jeki unyunyiziaji mashamba maji.

“ Tumetimiza masharti yote kufanikisha mradi huu,lakini Kaunti ya turkana imesalia nyuma,” aliongeza Munyes.

Aliongeza kwamba makataa ya uzalishaji mapipa elfu-80 ya mafuta kila siku kufikia mwaka 2022 yataahirishwa hadi mwaka 2023-2024 kutokana na janga la COVID 19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *