Mtu mmoja auawa na fisi, watatu wajeruhiwa huko Samburu

Mvulana mmoja ameaga dunia na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa na fisi katika eneo la Suguta Marmar, Kaunti ya Samburu.

Akithibitisha kisa hicho, Naibu Kamanda wa Polisi wa Samburu ya Kati Abdikadir Malicha amesema mvulana huyo amefariki wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti hiyo mjini Maralal.

Mvulana huyo alikuwa pamoja na dadake mdogo wa darasa la pili ambaye amepata majeraha ya miguuni na mikononi walipovamiwa na fisi huyo wakati walipokuwa wakichunga mifugo ya familia yao.

Kulingana na Malicha, watu wengine wawili waliojitokeza kuwanusuru watoto hao pia walijeruhiwa.

“Polisi walifika katika eneo la tukio na kuwapeleka jumla ya watu wanne hospitalini wakiwa na majeraha. Hata hivyo, mvulana mmoja akafariki wakati akipokea matibabu, mmoja bado anaendelea na matibabu hospitalini na wawili wakaruhusiwa kurudi nyumbani baada ya matibabu,” akasema.

Malicha pia amethibitisha kuwa wakazai walijitokeza na kukabiliana na fisi huyo hadi wakafanikiwa kumuua.

Wakazi hao sasa wanaiomba serikali kupitia kwa KWS kuimarisha juhudi za kuwalinda dhidi ya wanyama wa porini.

Wameitaka serikali pia iwalipe fidia walionusurika na uvamizi wa wanyama wa porini katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *