Msimu wa Krismasi ni changamoto kuu kwa msambao wa Covid-19

Waziri wa afya Mutahi Kagwe ameonya kwamba msimu wa sherehe za Krismasi huenda ukazidisha msambao wa virusi vya Covid-19, iwapo hatua za kudhibiti virusi hivyo hazitachukuliwa.

Kwa mujibu wa Kagwe, uvaliaji wa barakoa, unawaji mikono na uwekaji umbali ufaao, utasaidia kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo na hivyo kuokoa maisha.

“Tunapoingia katika msimu wa sherehe, tuwe makini zaidi kuhakikisha hatuko katika orodha aidha ya maafa au wale walioambukizwa virusi hivyo,” alisema waziri huyo.

Kagwe alisema hayo huku taifa hili likinakili visa 356 vipya vya Covid-19 na kufikisha jumla ya visa vya maambukizi humu nchini kuwa 93,761.

Waziri alisema visa hivyo vipya vilitokana na sampuli 5,768 zilizopimwa katika muda was aa 24 zilizopita.

Alisema wagonjwa 852 kwa sasa wamelazwa katika hospitali mbali mbali kote nchini na wengine 5,973 wako chini ya mpango wa kuwahudumia wagonjwa nyumbani.

Hata hivyo wagonjwa 11 zaidi wamefariki kutokana na ugonjwa huo na kufikisha jumla ya idadi ya waliofariki kuwa 1,629.

Wizara ya afya pia iliripoti kuwa wagonjwa 275 zaidi wamepona virusi hivyo na kufikisha 75,274 idadi jumla ya wale waliopona humu nchini.

Idadi hiyo mpya ya waliopona Covid-19, 227 walikuwa katika mpango wa kuwahudumia wagonjwa nyumbani huku 48 wakiruhusiwa kuondoka katika taasisi mbali mbali za afya kote nchini.

Kati ya visa hivyo vipya, 346 ni wakenya ilhali wagonjwa kumi ni raia wa kigeni.

Wagonjwa 227 ni wa kiume ilhali 129 ni wa kike huku aliye mchanga zaidi akiwa na mwaka mmoja na mzee zaidi akiwa na miaka 93.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *