Mshukiwa wa ugaidi akamatwa akipiga picha Kituo cha Polisi cha Makongeni

Maafisa wa Polisi wamemkamata mshukiwa mmoja wa ugaidi aliyepatikana akipiga picha Kituo cha Polisi cha Makongeni, Jijini Nairobi.

Mshukiwa huyo pia alikuwa anapiga picha gari ya polisi ya kituo hicho, yenye nambari ya usajili GK A 318.

Kulingana na taarifa ya polisi, Augustine Juma, mwenye umri wa miaka 34, alitiwa nguvuni na simu yake ya mkononi kuchukuliwa na maafisa hao kwa uchunguzi.

Maafisa walipotazama hifadhi ya simu hiyo, walipata picha za Benki Kuu ya Kenya, Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI), Ubalozi wa Israeli na Kituo cha Polisi cha Barabara ya Jogoo.

Aidha, maafisa hao wamepata picha za maafisa wengine wakipokea mafunzo mbali mbali, raia waliokamatwa na washukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, Mlolongo wa magari na watu waliojihami wanaokisiwa kuwa wa kundi hilo la Al-Shabaab na pia kanda ya video ya mshukiwa huyo akimtesa mtu asiyejulikana aliyekuwa amefungwa pingu mikononi.

Mshukiwa huyo amekamatwa na kupelekwa katika Makao Makuu ya APTU kwa hatua zaidi za kisheria.

Kufuatia visa vya kigaidi vinavyoripotiwa katika sehemu mbali mbali za nchi, serikali imeimarisha juhudi za kukabiliana na hali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *