Msako dhidi ya pombe haramu waimarishwa Makueni

Serikali imeanzisha msako dhidi ya uuzaji wa bangi na pombe haramu katika baadhi ya maeneo ya  Kaiti na  Mbooni katika kaunti ya Makueni.

Kamishna wa kaunti hiyo  Maalim Mohammed amesema kuwa msako huo ambao ulianza siku ya Jumanne usiku umeshuhudia kukamatwa kwa washukiwa watatu na kunaswa kwa lita 600 za pombe haramu inayofahamika kama Kaluvu katika lokesheni ya Iuani katika eneo la Kaiti.

Msako huo ulianzishwa kufuatia ufichuzi wa siku ya Jumanne katika jarida moja la humu nchini kuhusu kuuzwa kwa bangi na pombe haramu aina ya Kaluvu katika  vijiji vya  Iuani, Kyamuata, Mutula, Kithungo, Uthekeni, Kithangathini, Katulye na  Ngai.

Akihutubia mkutano wa baraza katika kanisa katoliki la  Ngai katika eneo la Kaiti, Maalim alisema kuwa msako huo utaendelea hadi magenge yanayolangua bangi na pombe hiyo haramu yakabiliwe na kuangamizwa.

“Tumetangaza vita dhidi ya pombe haramu aina ya Kaluvu. Msako huu utadumu hadi pale pombe haramu na bangi zitamalizwa kabisa. Wale wanaouza pombe hiyo haramu na bangi hawatakuwa na pahali pa kujificha,” alisema Maalim

Msako huo utaongozwa na maafisa wakuu wa vituo mbalimbali vya polisi, machifu na manaibu wa machifu katika maeneo yao husika.

Kamishna huyo wa kaunti alielezea wasiwasi kwamba kaunti ya makueni imeorodheshwa ya juu kwa utumizi wa pombe haramu na bangi huku akitoa wito wa juhudi za pamoja kutoka kwa wadau kukabiliana na tatizo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *