Morans wapakatwa na Angola michuano ya kufuzu kwa Fiba Afrobasket
Matumaini ya timu ya taifa ya Kenya katika mpira wa kikapu almaarufu the Morans kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao yalididimia baada ya kuambulia kichapo cha pointi 66-83 kutoka kwa Angola katika mechi ya pili ya kundi B ya kufuzu, iliyosakatwa Alhamisi Alasiri katika uwanja wa Kigali Rwanda.
Morans walipoteza robo ya kwanza ya mchezo pointi 10-18 na ya pili 15-21, lakini wakanyong’oyea zaidi katika robo ya tatu walipocharazwa alama 13-29.
Mabadiliko kadhaa ya kiufundi kutoka kwa kocha Cliff Owuor yaliimarisha mchezo wa Wakenya waliojizatiti na kunyakua ushindi katika kwota ya mwisho ya mchezo alama 28-15 ingawa tayari maji yalikuwa yamezidi unga.
Reuben Mutoro na Tyler Ongwae walikuwa wafungaji bora wa pointi kwa Kenya ,kila mmoja akizoa alama 18 .
Nahodha wa kenya Mutoro amesema walicheza vizuri dhidi ya Angola kuliko dhidi ya Senegal huku akiahidi kwamba wataimarisha mchezo wao zaidi dhidi ya Msumbiji Ijumaa “Tulicheza vyema katika mechi ya leo kinyume na mechi ya Jumatano ,naamini kuwa tutarudi kufanya utafiti na kujitayarisha vyema dhidi ya Msumbiji ambao nina imani tutaimarika zaidi na kupata ushindi”akasema Mutoro
“Kwetu sisi mechi ya Msumbiji ni kama fainali tutajituma kwa asilimia 100 kwani hatuna kingine cha kuhofia au kutuzuia na baada ya hapo tutangoja raundi ya pili mwaka ujao”akaongeza Mutoro
Kwa upande wake kocha Owuor amesema kuwa alijaribu kurekebisha makosa mengi waliyofanya dhidi ya Senegal ,walipochuana na Angola na ameahidi kwamba analenga ushindi katika mechi ya mwisho Ijumaa dhidi ya Msumbiji kabla ya kurejea kwa raundi ya pili Februari mwaka ujao.
”Tumekuwa na makosa mengi uwanjani ,ukiangalia tumekuwa tukipoteza mpira kwa urahisi na pia walinzi wetu hawajamakinika ipasavyo,lakini nafurahia mchuano wetu wa leo umekuwa bora kuliko ule dhidi ya Senegal.Kwa sasa tunajiandaa kucheza na Msumbiji tutafute matokeo bora halafu turejee tena Februari mwaka ujao kwa raundi ya pili”akasema kocha Owour
Ushinde wa Morans dhidi ya Angola ulikuwa wa pili mtawalia katika kundi B kwenye mashindano hayo ,baada ya kulazwa pointi 54-97 katika pambano la ufunguzi siku ya Jumatano.
Hii ina maana kuwa Kenya ni sharti waishinde Msumbiji katika mchuano wa mwisho Ijumaa hii kuanzia saa kumi na mbili jioni ,ili kuwa na fursa ya kutinga mashindano ya Fiba Afrobasket mwakani nchini Rwanda.
Angola wanaongoza kundi hilo baada ya kushinda mechi ya pili walipowaangusha Msumbiji Jumatano usiku katika mechi ya kwanza.
Katika mechi ya pili Alhamisi Nigeria imeibwaga Sudan Kusini pointi 76-56 katika kundi D.
Mkondo wa kwanza wa mechi za makundi utakamilika Jumapili ijayo kabla ya mkondo wa pili kuanza Februari 19 mwaka ujao.
Timu tatu bora kutoka kila kundi baada ya mechi 6 za makundi zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.