Morans wa kenya kufungua kipute cha Fiba Afrobasket dhidi ya Senegal Jumatano
Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ‘Morans’ itachuana na Senegal Jumatano kuanzia saa kumi na mbili jioni katika mechi ya ufunguzi ya kundi B kwenye michuano ya kufuzu kwa mashindano ya kombe la bara Afrika mwaka ujao maarufu kama Fiba Afrobasket mjini Kigali, Rwanda.
Katika mchuano mwingine wa pili wa kundi B Jumatano ,Msumbiji watashuka uwanjani saa tatu usiku kupambana na Angola.
Morans baade watachuana na Angola Alhamisi na kisha kuhitimisha ratiba ya kundi B Ijumaa dhidi ya Msumbiji.

Kenya ilifuzu kwa mechi hizo baada ya kuwashinda Sudan Kusini kwenye mechi ya mwisho ya kufuzu mwaka jana hapa Nairobi.
Morans inayonolewa na mwalimu Cliff Owuor ilikuwa imesajili ushindi wa wa pointi 68-66 dhidi Sudan Kusini katika pambano la kujipiga msasa lililoandaliwa Jumanne mjini Kigali.
Mataifa 20 yaliyotengwa katika makundi matano yanashiriki mashindano hayo huku mabingwa watetezi Tunisia wakijumuishwa kundi A pamoja na Jamhuri ya Afrika ya kati, Madagascar na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
Wenyeji Rwanda wamerundikwa kundi C pamoja na Nigeria, Mali na Algeria, ilihali kundi E linashirikisha Misri, Morocco, Uganda na Cape Verde.
Mataifa matatu bora kutoka kila kundi yatafuzu kwa mashindano ya kuwania kombe la bara Afrika mwaka ujao mjini Kigali Rwanda .

Kufikia sasa mataifa ya Cameroon, Kodivaa na Equatorial Guinea yamejikatia tiketi kwa kipute cha mwakani .
Pata uhondo wote wa mechi za Morans kupitia runinga ya taifa KBC Channel one baina ya Jumatatno na Ijumaa hii.