Moji Short Baba afanya harusi

Harusi ya mwimbaji huyo wa nyimbo za kisasa za injili ilifanyika wikendi ambayo imepita, wiki chache tu baada ya kumchumbia mpenzi wake Nyawira Gachugi ambaye sasa ni mke wake.

Harusi ya wawili hao ilifichwa kutoka kwa jicho la umma na ilijulikana tu jana pale ambapo wanandoa hao walichapisha picha za harusi.

Moji ambaye jina lake halisi ni James Muhia alipachika picha hizo akisema amekuwa akisubiri fursa ya kutumia maneno ya Biblia; “Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana” kutoka kitabu cha Mithali 18:22.

“Nyawira Gachugi nafurahi nilikupata na ninasubiria kwa hamu kuona aliyotuandalia Mungu” aliendelea kusema mwimbaji huyo.

Nyawira naye alipachika picha za harusi kwenye Instagram akisema sasa amekuwa mke wa mtu na anafurahia kwamba ‘milele’ yake imeanza.

Moji Short Baba alianza kuimba katika kundi la watu wawili kwa jina “Kelele Takatifu” kabla ya kundi lenyewe kusambaratika miaka kama mitatu iliyopita.

Baadaye yeye na mwenzake Silvanus Otieno maarufu kama Didi walianza kuimba kila mmoja kivyake.

Ana nyimbo nyingi ambazo zinapendelewa sana na vijana kama vile Mazuri akimshirikisha Guardian Angel, Dance Ya Kanisa, Mungu Wa Musa, Wacha Kunicheki, Unabore, Imani,Yesu Mtaani na One Day.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *