Mohamed Bazoum atangazwa kuwa Rais mpya wa Niger

Tume ya uchaguzi Nchini Niger imemtangaza mgombea wa chama kinachotawala nchini humo, Mohamed Bazoum, mshindi wa marudio ya uchaguzi wa urais.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI), Issaka Souna, alitangaza kuwa Bazoum amepata asilimia 55.75 ya kura zilizopigwa mnamo Februari 21.

Bazoum alimshinda rais wa zamani Mahamane Ousmane ambaye alipata asilimia 44.25 ya kura hizo.

Kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mnamo tarehe 27 Disemba mwaka uliopita, Bazoum aliongoza matokeo kwa kupata asilimia 39 ya kura hizo huku Ousmane akimfuata kwa takriban asilimia 17 ya kura.

Mapema Jumanne, waendeshaji kampeni wa Ousmane walidai udanganyifu ulitokea pamoja na wizi na pia visa vya kujazwa kwa masanduku ya kura na vitisho dhidi ya wapiga kura bila kutoa ushahidi.

Rais anayeondoka Mahamadou Issoufou anang’atuka madarakani kwa hiari baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kushuhudia kupokezana madaraka kati ya viongozi wawili waliochaguliwa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1960.

Taifa hilo limeshuhudia mashambulizi kutoka kwa makundi ya kigaidi yaliyojihami kutoka nchi jirani za Mali na Nigeria.

Siku ya marudio ya kura hizo, maafisa saba wa tume ya CENI waliaga dunia baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa ardhini Magharibi mwa eneo la Tillaberi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *