Categories
Burudani

Mlinzi wa Bobi Wine auawa

Mmoja wa walinzi wa mwanamuziki wa Uganda Bobi Wine anasemekana kuaga dunia baada ya kugongwa na lori la polisi katika eneo la Busega.

Francis Ssenteza Kalibala ambaye ni mlinzi wa binafsi wa Bobi Wine mwaniaji urais wa chama cha National Unity Platform NUP, anasemekana kugongwa na gari hilo la polisi wakati kundi la kampeni la Bobi lilikuwa njiani kutoka eneo la Masaka kuelekea jiji kuu Kampala kwa ajili ya kutafutia mwanahabari matibabu zaidi.

Lori hilo la polisi nchini Uganda ambalo nambari ya usajili ni “H4DF 2382” linasemekana kutumika kuzuia msafara wa Bobi Wine uliokuwa katika eneo hilo ukijaribu kuokoa maisha ya mwanahabari.

Mwanahabari huyo wa Ghetto Media kwa jina Ashraf Kasirye naye anasemekana kupigwa risasi kichwani na polisi wakati kundi la kampeni la NUP lilikuwa likielekea Lwengo kwa ajili ya kampeni za siku ya leo.

Francis anasemekana kuaga dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Lubaga. Kufikia sasa hakuna taarifa kuhusu mwanahabari Ashraf aliyepigwa risasi.

Kampeni za Bobi Wine mbunge wa Kyandondo mashariki kwa jina halisi Robert Ssentamu Kyagulanyi huwa zinaingiliwa kila mara na maafisa wa usalama nchini Uganda.

Kwa wakati mmoja Bobi Wine alikamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid 19 jambo ambalo lilizua ghasia na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Yeye ndiye mpinzani wa karibu wa Rais wa sasa nchini Uganda Yoweri Kaguta Museveni kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ingawaje kuna wawaniaji wengine wengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *