Mkutano wa IGAD kuhusu miundo msingi wang’oa nanga Nairobi

Mkutano wa pili wa kujadili mpango wa ustawishaji miundo msingi wa Shirika la IGAD umeanza jijini Nairobi huku miito ikitolewa ya kushughulikia masuala ya vijana.

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi, Balozi Moi Lemoshira kutoka Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni amesema mpango huo umewezesha kupigwa kwa hatua kadhaa za kuhakikisha ufanisi wa biashara huru Barani Afrika.

Lemoshira ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo wa siku mbili kutoa mapendekezo ya kushughulikia masuala mbali mbali ya vijana hasa kuhusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Mkurugenzi Mkuu wa IGAD Workneh Gebeyahu amewahimiza washiriki wa mkutano huo kujadilia sekta nne kuu za mpango huo zikiwemo uchukuzi, kawi, teknolojia ya habari na mawasiliano na maji ya mito inayopitia mataifa kadhaa.

Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa ushirikiano wa kiuchumi wa IGAD Elsadig Abdalla, Gebeyahu amesema hatua hiyo imewadia wakati mwafaka ambapo IGAD inatayarisha mpango wa pili wa ustawishaji miundo msingi na ajenda ya maendeleo Barani Afrika ya mwaka wa 2063.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *