Mjue Mpinzani Mkuu wa Magufuli, Tundu Lissu, kwenye uchaguzi wa urais Tanzania

Uchaguzi mkuu wa Tanzania 2020, utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba, unatarajiwa kushuhudiwa ushindani mkubwa katika kinyang’anyiro cha urais nchini humo.

Rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli anaazimia kuchaguliwa kwa awamu ya pili kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, CCM, ambacho kimekuwa uongozini tangu mwaka wa 1977.

Hata hivyo, Magufuli anacho kibarua kigumu atakapokabiliana na mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, Tundu Lissu.

Je, mgombea huyu ni nani?

Tundu Antiphas Mughwai Lissu alizaliwa tarehe 20 Januari mwaka wa 1968, akiwa na umri wa miaka 52 sasa.

Ni mkazi-asili wa eneo la Singida lililoko umbali wa takribani maili 200 Kaskazini-Magharibi mwa mji mkuu wa Dodoma.

Tundu Lissu ni Mwanasheria ambaye kutokana na ushupavu wake katika taaluma hiyo, alichaguliwa katika wadhifa wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania na pia Mwanasheria Mkuu wa chama cha Chadema.

Lissu alianza kupata umaarufu katika ulingo wa siasa alipogombea kiti cha ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka wa 2010 na kufaulu katika uchaguzi huo kwa tiketi ya Chadema.

Lissu anatajwa kama mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, asiyeogopa kukosoa serikali na hasa Rais Magufuli, ambaye ameonekana kutofautiana naye tangu kuchaguliwa kwake mwaka wa 2015.

Kutokana na msimamo wake mkali na matamshi ya kuupinga uongozi wa nchi hiyo, Lissu amepitia masaibu mengi ukiwemo msururu ya visa vya kukamatwa kwake na kushtakiwa kwa madai ya uchochezi miongoni mwa mashtaka mengine mengi.

Mnamo tarehe saba Septemba mwaka wa 2017, genge la watu wasiojulikana lilimvamia Tundu Lissu nyumbani kwake Dodoma na kumjeruhi vibaya kwa kumpiga risasi mara kadhaa mwili mzima.

Kufuatia kisa hicho, viongozi na wafuasi wa upinzani nchini Tanzania waliulaumu utawala wa nchi hiyo, wakiukashifu kwa uwezekano wa kuhusika katika kitendi hicho.

Hata hivyo, Rais Magufuli alijitokeza na kushtumu kitendo hicho mbali na kuagiza uchunguzi ufanywe ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria lakini hadi sasa, hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kukamatwa kufuatia kisa hicho.

Lissu alikimbizwa hadi Hospitali Kuu ya Dodoma alikopokea matibabu ya dharura kwa masaa machache kabla kusafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Aga Khan katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.

Alitibiwa kwa miezi kadhaa kabla kusafirishwa tena hadi nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ya kuimarisha viungo vyake ambako anasemekana kufanyiwa upasuaji mara 19 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg.

Mnamo Julai mwaka huu, Tundu Lissu alirejea nchini Tanzania na kupokelewa na umati mkubwa wa wafuasi wake, ujio ambao ulipandisha joto la siasa za uchaguzi wa urais nchini humo.

Tarehe tatu Agosti 2020, wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema walipiga kura ya kumtafuta mgombea wa chama hicho atakayekabiliana na Rais Magufuli katika kinyang’anyiro cha urais.

Kamati kuu ya Chadema ilikuwa imeidhinisha majina ya wagombea watatu ambao walipigiwa kura ya mchujo.

Tundu Lissu aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 405 kati ya 442 zilizopigwa, na kuwapiku wagombea wenza Lazaro Nyalandu aliyepata kura 36 na Dkt. Mayrose Majige aliyepata kura moja.

Kufuatia matokeo hayo basi, Tundu Lissu alitangazwa kama mgombea atakayepeperusha bendera ya Chadema.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa nchini humo, uteuzi wa Lissu kukabiliana na Magufuli ulitokana na msimamo wake mkali wa kisiasa.

Chama hicho kilikuwa na nia ya kurudisha imani ya wafuasi wake baada ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho kuhamia chama tawala kinachoongozwa na Magufuli baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2015.

Aliyekuwa mgombea wa Chadema katika uchaguzi huo wa uraisi Edward Lowassa pia alihamia CCM baada ya kushindwa na Magufuli, hatua iliyowaghadhabisha wafuasi wa Chadema.

Kampeni za kuelekea uchaguzi wa mwaka huu zilipamba moto, huku Rais Magufuli akiwahakikishia wananchi wa Tanzania maendeleo zaidi katika awamu ya pili iwapo watamchagua tena.

Naye Lissu amepata umaarufu mkubwa hasa miongoni mwa vijana, akiahidi kuinua uchumi wa nchi hiyo, kuongeza mishahara kwa wahudumu wa sekta ya umma, kuwafidia waliomizwa na serikali iliyo mamlakani na kuanzisha mchakato wa mageuzi ya katiba ndani ya siku 100 za kwanza uongozini.

Hata hivyo, masiabu ya Lissu yalianza kumkabili tena mwishoni mwa mwezi jana alipotakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi nchini humo baada ya kusikika akisema tume hiyo ina njama ya kuiba kura za urais kwa faida ya Magufuli.

Juma moja baadaye, Lissu alipewa adhabu ya marufuku ya kutofanya kampeni kwa siku saba zilizofuata baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi kwenye mojawapo ya mikutano yake ya kampeni.

Huku wananchi wa Tanzania wakielekea debeni Jumatano, kitendawili kilichopo ni iwapo Tundu Lissu ataweza kumbwaga Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuandikisha historia ya kuking’atua madarakani chama tawala cha CCM ambacho kimeongoza taifa hilo tangu kuundwa kwake mwaka wa 1977.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *