Mitch McConnell akosoa wito wa Trump kuhusu msaada kwa waathiriwa wa COVID-19 Marekani

Kiongozi wa chama cha Republican kwenye Bunge la Seneti nchini Marekani Mitch McConnell, amepuuzilia mbali wito wa kuongezwa kwa misaada kwa waathiriwa na janga la Corona.

Wito huo unashinikizwa na Rais Donald Trump, wajumbe wa chama cha Democratic na pia baadhi ya wanachama wa Republican.

McConnell amesema pendekezo la kuongeza misaada hiyo kutoka dola 600 hadi 2,000 kwa kila mwathiriwa itakuwa njia nyengine ya ufujaji wa fedha.

Bunge la Congress lililo na wafuasi wengi wa chama cha Democratic lilikuwa limepiga kura kuongeza misaada ya kuwanusuru raia wa Marekani kutokana na athari za janga la COVID-19.

Mwingilio wa Rais huyo anayeondoka umewagawanya wafuasi wa chama chake cha Republican.

Bunge la Congress lilikuwa limeidhinisha ruzuku ya dola 600 kwa kila muathiriwa wa janga la hilo na pia mswaada kuhusu ufadhili wa serikali ambao Rais Trump aliurejesha bungeni kabla ya siku ya Kristmasi, akisema waathiriwa hao wanapaswa kulipwa fedha nyingi zaidi.

Siku ya Jumatatu, wajumbe wa chama cha Democratic kwenye Bunge la Congress, ambao kwa kawaida huwa mahasimu wa kisiasa wa Rais Trump, waliidhinisha pendekezo lake la malipo ya dola 2,000 kwa kila mhasiriwa.

Wajumbe kadhaa wa chama cha Republican, ambao hawangetaka kuonekana wakimpinga Rais huyo, waliungana na wenzao wa chama cha Democratic katika kuidhinisha malipo hayo.

Ijapo kwa shingo upande, Trump alitia saini mswaada wa awali na kuufanya sheria siku ya Jumapili, lakini hajaacha kuitisha fedha nyingi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *