Migodi yafungwa Kwale kwa tishio la kiusalama

Halmashauri ya Usimamizi wa Mazingira nchini NEMA imesitisha kwa muda shughuli katika baadhi ya migodi ya Kunti ya Kwale kutokana na hatari za kiafya na usalama wa wafanyikazi.

Juma lililopita, watu wawili walifariki na wengine kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na jiwe kubwa walipokuwa wakifanya kazi katika Mgodi wa Maweni katika eneo la Ukunda, Kaunti Ndogo ya Msambweni.

Kabla ya kisa hicho, mwanamke mmoja aliripotiwa kufunikwa hadi kufariki alipokuwa akifanya kazi mgodini hapo miezi miwili iliyopita.

Kamishna wa Kaunti ya Kwale Karuku Ngumo amesema kuwa kufungwa kwa migodi hiyo kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka husika kufanya uchunguzi na kutoa muongozo mwafaka wa shughuli hizo.

“Tunafunga migodi hii kwa muda mpaka maswala ya usalama yaangaziwe,” amesema Ngumo, huku akitoa agizo la wamiliki wa migodi hiyo kusitisha shughuli za uchimbaji mara moja.

Ngumo amesema migodi hiyo imekuwa tishio kwa wafanyikazi wake na pia inaathiri afya za wakazi wanaoishi karibu.

Mkurugenzi wa NEMA, tawi la Kwale Geoffrey Wafula na Mwanajiolojia Fredrick Wafula pia wamefanya ziara katika migodi hiyo na kuahidi kuchunguza migodi yote katika Ukanda wa Pwani.

Wakuu wa NEMA pia wamewalaumu wamiliki wa migodi midogo midogo katika eneo hilo kwa uharibifu wa ardhi na kushindwa kufukia mashimo baada ya shughuli zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *