Mgomo wa Wauguzi nchini waanza

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) kimesisitiza kwamba mgomo wao uliopangwa kuanza Jumatatu bado ungalipo.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako, amesema kipindi cha makataa ya mgomo wao kilimalizika Jumapili na wameanza mgomo leo hadi kutimizwa kwa matakwa yao.

“Mgomo kote nchini uliopangwa kuanza Jumatatu tarehe saba Desemba, 2020, bado ungalipo. Tunawahimiza wanachama wetu waungane tunapotetea haki zetu,” amesema Panyako.

Panyako amesema swala la pekee ambalo limeshughulikiwa kwa kiwango fulani ni kutangazwa kwa janga la COVID-19 kuwa hatari kwa afya.

Ameweaagiza maafisa katika matawi yote kushiriki na kuhakikisha ufanisi wa mgomo huo.

Miongoni mwa maswala yanayoibuliwa na chama hicho cha wauguzi ni pamoja na kuwalipa wauguzi wote shilingi elfu 30 kama marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira hatari, wauguzi wote kulipwa fedha zote za mishahara na pia fedha walizokatwa kuwasilishwa kwa taasisi husika.

Pia wanataka wauguzi wote vibarua kuajiriwa kwa masharti ya kudumu na kuajiriwa kwa wauguzi elfu saba zaidi ili kusaidia katika vita dhidi ya COVID-19.

Chama hicho kinataka wauguzi kupewa vifaa vya kutosha vya kujikinga kwani wao hua wa kwanza kukutana na wagonjwa wanapowasili kwenye taasisi za afya.

Aidha, wauguzi wanataka kukamilika kwa mkataba wa pamoja kuhusu nyongeza ya mishahara.

Wanataka pia kuwepo mpango makhsusi wa bima ya matibabu kwa wauguzi kutokana na magonjwa yote ukiwemo ule wa COVID-19 na kufidiwa haraka kwa familia za zaidi ya wauguzi 18 ambao hadi sasa wamefariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Pia wanataka kujumuishwa kwa pendekezo la kubuni Tume ya Kuajiri wahudumu wa sekta ya afya miongoni mwa mapendekezo mengine ya mpango wa BBI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *