Mgomo wa wahudumu wa afya kuanza usiku wa manane

Huduma za afya kwenye hospitali za umma huenda zikalemazwa kuanzia usiku wa manane ikiwa wahudumu wa afya watatekeleza tisho lao la kugoma baada ya kumalizika kwa makataa yao ya siku 21.

Katika kile ambacho huenda kikaashiria msukosuko kwenye Sekta ya Afya, wahudumu wa afya wamedumisha msimamo wao baada ya mashauriano baina yao na serikali kugonga mwamba.

Wakati wa kutoa ilani zao mnamo tarehe tofauti chama cha wahudumu wa sekta ya afya na wataalamu wa tiba ya meno, Chama cha kitaifa cha matabibu na pia chama cha kitaifa cha wauguzi viliitaka serikali kuwahakikishia usalama wao wa mahala pa kazi, kufuatia janga la COVID-19.

Hilo lilikuwa jaribio la tatu tangu mwezi Mei la wahudumu wa sekta ya afya kugoma lakini migomo yao imekuwa ikiahirishwa.

Miongoni mwa masuala yanayozozaniwa, ni pamoja na kuwapa vifaa vya kutosha vya kujikinga, Maafisa wote walioorodheshwa miongoni mwa makundi ya walio hatarini kutojumuishwa katika majukumu ya mstari wa mbele, Kuwepo mpango makhsusi wa bima ya matibabu, Kupandishwa vyeo, kuorodheshwa kulingana na majukumu yao, Kuwianishwa kwa marupurupu yao ya kufanya kazi katika mazingira hatari na pia kubuniwa kamati ya taasisi mbali mbali kuchunguza malalamishi yao.

Zaidi ya wahudumu 30 wa afya wameaga dunia kufikia sasa kutokana na maambukizi ya virusi vya korona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *