Mgomo wa madaktari sasa wanukia

Huduma kwenye Sekta ya Afya huenda zikasambaratika kuanzia usiku wa manane endapo madaktari ambao ni wanachama wa Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno, KMPDU, watatekeleza tishio lao la kugoma.

Madaktari hao wamesema kuwa mazungumzo baina yao na serikali yamegonga mwamba na hivyo watajiunga na wauguzi na matabibu ambao walianza mgomo wao wiki mbili zilizopita.

Madaktari wanaotarajiwa kugoma ni pamoja na wataalamu wa matibabu, madaktari wa meno, wakurugenzi wa afya katika kaunti, wataalamu wa dawa na madaktari walio mafunzoni.

Wahudumu hao hawatafika kazini kesho baada ya mazungumzo kuvurujika walipoahirisha mgomo wao kwa siku 14.

Mgomo wa madaktari huenda ukasadifiana na ule wa wauguzi na matabibu ambao umedumu kwa siku 14.

Maafisa wa matibabu wamedumisha kuwa wataendelea na mgomo wao licha ya onyo la Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, kwamba watafutwa kazi kwa kukaidi agizo la mahakama la kuwataka warudi kazini.

Wahudumu wa afya wamegoma ili kushinikiza wapewe vifaa bora vya kujikinga na maambukizi, wale walio na changamoto fulani wasiwe kwenye msitari wa mbele, wawe na bima kamili ya matibabu, kuwalipa mshahara wahudumu waliopelekwa katika serikali za kaunti chini ya mpango wa afya kwa wote na kuwianishwa kwa marupurupu ya kuhudumu katika mazingira hatari, miongoni mwa matakwa mengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *