Mfanyikazi wa KBC aliyeuawa Betty Barasa kuzikwa leo alasiri

Mhariri Mwandamizi wa video katika Shirika la Utangazaji humu nchini KBC, mareehmu Betty Mutekhele Barasa atazikwa leo alasiri nyumbani kwake katika eneo la Oloolua, Ngong, Kaunti ya Kajiado.

Awali, ibada ya wafu iliandaliwa katika makazi ya kuomboleza ya Montezuma, Jijini Nairobi, ikiongozwa na Baba Micah Kemboi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la KBC Dkt. Naim Bilal alimpongeza marehemu Bi. Barasa kama mfanyikazi aliyetia bidii kamili katika majukumu yake.

Katika hotuba yake, Naibu Meneja wa maswala ya wafanyikazi katika shirika hilo Pamela Mogaka, kwa niaba ya Dkt. Bilal, alisema kwamba Betty alihudumia shirika hilo kwa uadilifu, alikuwa rafiki wa wengi na daima alikuwa tayari kuchukua majukumu yoyote.

Mumewe Betty, Geoffrey Namachanja, alimpongeza mkewe mpendwa kama mama wa dhati. Alisema amepoteza nguzo aliyotegemea kwa kila hali, ikiwemo hali ya kifedha na pia kwa njia nyingine nyingi kwa kipindi cha miaka 17 iliyopota.

Marafiki na watu wa familia ambao walihudhuria ibada hiyo ya wafu ni akiwemo Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Wanyama Musiambo, Seneta wa Bungoma Moses Wetangula na Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga.

Walihimiza polisi kuharakisha uchunguzi kufuatia mauaji ya Betty na kuhakikisha kwamba wahusika wote wanafikishwa mahakamani .

Kwa upande wake, Wanyama Musiambo aliihakikishia familia na waombolezaji wote kwamba serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba waliohusika na mauaji hayo wanafikishwa mahakamani.

Betty Barasa aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi nyumbani kwake siku ya Jumatano Juma lililopita.

Amemuacha Mume , Geoffrey Barasa na watoto watatu.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *