Mercy Johnson apendeza kwenye hafla ya kuwekwa wakfu kwa mtoto wake

Muigizaji wa nchi ya Nigeria Mercy Johnson anajulikana kwa umbo lake zuri la kiafrika ambalo yeye huambatanisha na mavazi ya kupendeza.

Mercy alijifungua mtoto huyo kwa jina ‘Divine-Mercy’ mwezi wa tano mwaka huu wa 2020, huko Marekani na wakati uliwadia wa kumweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo ni la kawaida kwa wakristo.

Mwanadada huyo alitikisa mitandao ya kijamii na picha za familia yake kuhusu tukio hilo ambapo alivaa vazi la kupendeza la rangi nyekundu rangi ambayo wote walikuwa wamevalia. Aliandika, “Tuliweka wakfu zawadi ya Mungu kwetu.”

Kulingana na maelezo kwenye akaunti yake ya Instagram, nguo aliyovalia Mercy Johnson ilishonwa na mwanamitindo maarufu Abiodun Shade Sandra ambaye anamiliki kampuni kwa jina “luminee couture” ambayo huvisha watu wengi maarufu nchini Nigeria.

Alimsifia sana mwanamitindo huyo akisema kwamba akiamua kushona nguo hana mchezo. Haijulikani kama mavazi ya watoto na baba yao pia yalishonwa na mwanamitindo huyo.

Mercy Johnson na mume wake Prince Odianosen Okojie walifunga ndoa mwaka 2011 na sasa wana watoto wanne.

Mwezi Novemba Mwaka 2013 Mercy Johnson alipigwa marufuku kuigiza nchini Nigeria baada ya watayarishaji filamu kulalamika kwamba alikuwa amekuwa ghali mno.

Hata hivyo marufuku hiyo iliondolewa mwezi Machi mwaka 2014 kufuatia hatua yake ya kuomba msamaha. Kwa sasa mwanadada huyo ni kati ya waigizaji wanaolipwa hela nyingi mno kwenye filamu za Nollywood.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *