Meli ya mizigo ya Iran yalipuliwa katika pwani ya Yemen

Mlipuko umeharibu meli ya kusafirisha shehena iliyotia nanga kwenye pwani ya Yemen katika bahari ya shamu ambayo inadaiwa kutumiwa na kundi la Revolutionary Guards kufanya ujasusi.

Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Iran. Hatibu wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Iran,Saeed Khatibzadeh, alisema mlipuko huo uliolenga meli ya Saviz siku ya Jumanne, haukusababisha majeruhi yoyote na kisa hicho kinachunguzwa.

Alisema meli ya Saviz isio ya shughuli za kijeshi, ilikuwa ikisaidia kudumisha usalama ili kukabiliana na maharamia.

Maafisa wa Iran hawajalaumu pande yoyote kwa mlipuko huo, lakini jarida la New York Times lilimnukuu afisa wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa, akisema Israeli ilifahamisha Marekani kwamba vikosi vyake vilishambulia meli hiyo.

Afisa huyo alisema meli ya Saviz iliharibiwa upande wa chini na Israeli ilitekeleza shambulizi la kulipiza kisasi kufuatia shambulizi la awali la Iran dhidi ya meli za Israeli.

Maafisa wa Iran hawakutoa maoni kuhusu matamshi hayo ya Israeli, lakini waziri mkuu, Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne, aliwaambia wabunge wa chama chake cha Likud kwamba Israeli sharti iendelee kukabiliana na vitisho vya Iran vya kuzusha vita katika eneo la mashariki ya kati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *