Mbunge wa Tiaty William Kamket aachiliwa huru

Mbunge wa Tiaty William Kamket ameachiliwa huru kwa dhamana ya polisi ya pesa taslimu saa chache baada ya kukamatwa jijini Nairobi na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kileleshwa.

Hata hivyo mbunge huyo ameagizwa kufika katika afisi za idara ya upelelezi wa jinai katika kaunti ya Nakuru siku ya Jumanne wiki ijayo.

Kukamatwa kwake kulijiri siku chache baada ya waziri wa usalama wa kitaifa Dkt. Fred Matiangi kusema serikali inawasaka viongozi wanaoaminika kuhusika katika visa vya utovu wa usalama vilivyoripotiwa hivi majuzi katika kaunti ya Baringo.

Mbunge huyo wa chama cha KANU alikamatwa kwa madai ya kuhusika katika visa vya utovu wa usalama katika eneo la  Kapedo, kaunti ya Baringo.

Msako mkali ulizinduliwa  na serikali ili kusaka majambazi waliovamia maafisa wa usalama Jumapili na kusababisha kifo cha afisa mkuu wa kitengo cha GSU.

Maafisa wengine watatu waliuguza majeraha ya risasi wakati wa kisa hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *