Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ameachiliwa huru kwa dhamana

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki tano pesa taslimu na mahakama kuu ya Nakuru.

Jaji Joel Ngugi amesema sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka za kumzuilia kwa siku saba zaidi hazikutimiza masharti ya kukubaliwa.

Aidha jaji huyo amesema mbunge huyo hakustahili kukamatwa.

Ameshangaa ni kwa nini polisi walimkamata bila maelezo tangulizi ya uhalifu anaodaiwa kutekeleza.

Ngugi, hata hivyo amemzuia mbunge huyo kuhutubia mikutano ya hadhara.

Mnamo Jumatano hakimu mkuu wa mahakama ya  Nakuru  Josephat Kalo, alipuzilia mbali ombi la upande wa mashtaka la kumzuilia Sudi kwa siku 14.

Mbunge huyo siku ya Alhamisi jioni aliwasilisha ombi katika mahakama kuu mjini Nakuru akitaka kubatilisha uamuzi wa hakimu mkuu Josephat Kalo wa kumzuilia kwa siku saba kusubiri uchunguzi wa mashtaka matano yanayomkabili.

Hakimu mkuu Josephat Kalo aliagiza kuzuiliwa kwa mbunge huyo kwa wiki moja katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru kwa misingi kuwa akiachiliwa atavuruga amani na usalama wa umma.

Kuzuiliwa kwake pia kulilenga kuwapa polisi fursa ya kukamilisha uchunguzi wa madai ya matamshi ya uchochezi, mwendendo wa kukera, umiliki wa bunduki kinyume cha sheria miongoni mwa madai mengine.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *