Mbunge wa Jomvu ashtumu uhamisho wa Naibu Kamishna wa Kaunti

Mbunge wa eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa Badi Twalib ameiomba serikali kukoma kuwahamisha mara kwa mara Manaibu Kamishna wa Kaunti katika eneo bunge lake.

Kulingana na mbunge huyo, uhamisho huo wa mara kwa mara umeathiri pakubwa utendakazi wao na utoaji huduma kwa wananchi.

Twalib amehoji kwamba maafisa hao wa serikali wanapaswa kupewa muda wa kuzoea eneo hilo na kuyatambua matatizo yanayowakumba wakazi kabla kumakinika katika utendakazi wao.

“Kiongozi kutoa huduma ni yule kiongozi anayeweza kukaa hapa akaielewa hali ya Jomvu, akaelewa watu wa Jomvu wana shida gani akawasaidia,” amesema.

Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Mikindani kwenye mkutano wa kutoa hundi za Hazina ya Uwezo kwa akina mama na vijana wa eneo bunge lake.

Twalib amewapa changamoto vijana wajitokeze kwa wingi na kutuma maombi ya kufaidika na hazina hiyo.

Amehoji kwamba wengi wa wanaofanya hivyo ni makundi ya akina mama huku vijana wakikosa kujihusisha kikamilifu.

“Kwa hivyo nawasihi vijana wa sehemu yangu wajitolee kuja kuomba hizi pesa ili tuwapatie pesa wafanye biashara,” amesihi.

Jumla ya makundi 38 yamenufaika kutokana na hazina hiyo ambapo hundi za jumla ya shilingi milioni nne ziligawanywa kwa makundi hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *