Mbunge Oscar Sudi kuzuiliwa korokoroni siku mbili zaidi

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amezuiliwa kwa siku mbili zaidi kusubiri uamuzi wa kuachiliwa kwa dhamana kwenye kesi ambapo anatuhumiwa kwa kutoa matamshi ya chuki na uchochezi.

Sudi alifikishwa siku ya Jumatatu katika mahakama ya Nakuru ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la kumzuilia mbunge huyo kwa siku 14 kusubiri kukamilishwa kwa uchunguzi wa mashtaka dhidi yake.

Kulingana na hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani na upande wa mashatka, Sudi anakabiliwa na mashtaka ya kutoa matamshi ya chuki, kumshambulia afisa wa polisi, mienendo ya kukasirisha, kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria na kukataa kukamatwa.

Upande wa  mashtaka umesema unahitaji muda zaidi kutafuta na kuwahoji mashahidi kadhaa ambao unanuia kutumia ushahidi wao kwenye kesi hiyo.

Upande wa mashtaka pia unamtaka mbunge huyo wa Kapseret kuwasilisha bunduki aina ya Ceska iliyokuwa na risasi 11 ambayo ilipatikana ndani ya gari iliyokuwa katika makao yake.

Hakimu mkuu wa Nakuru Josephat Kalo ataamua kuhusu ombi hilo la upande wa mashtaka siku ya Jumatano wiki hii.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *