Matiang’i awaonya wanasiasa wachochezi

Waziri wa usalama wa Kitaifa Dkt. Fred Matiang’i amewatahadharisha wanasiasa dhidi ya kuwachochea Wakenya kuzua ghasia za kisiasa huku nchi hii inapokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Matiang’i amewahimiza wanasiasa kuwaheshimu Wakenya na kujiepusha na siasa za migawanyiko.

Akiongea katika Kaunti ya Nyamira, Waziri amesema wakati umewadia kwa viongozi kuepuka kutoa matamshi kiholela na siasa za kujitakia makuu.

Amesema hayo siku chache baada ya kukamatwa kwa Seneta wa Nandi Samson Cherargei, Mbunge wa Kimilili Didmas Barasa, Wilson Kogo wa Chesumei na Nelson Koech wa Belgut kwa madai ya kuwa na silaha na kwa kuzusha ghasia kwenye uchaguzi mdogo wa Kabuchai.

Kwa upande wao wabunge kadhaa wameishutumu Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kwa kile walichokitaja kuwa hatua kali zisizofaa za kuwataka wanasiasa kumi kuandikisha taarifa kuhusiana na kasoro za uchaguzi na ghasia.

Viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria wameitaka tume hiyo izuie visa kama hivyo badala ya kuwachukulia hatua wanaoshukiwa kuhusika navyo.

Kuria na mwenzake wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru wamesema mfumo wa sasa wa kisheria hauipi tume hiyo uwezo wa kuchukua hatua.

Waliongea wakati wa ibada ya Jumapili na harambee katika Kanisa la PCEA Macedonia Kayole jijini Nairobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *