Matiang’i aagiza kukamatwa kwa wazee wapenda ndogo ndogo

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Fred Matiang’i ameagiza kukamatwa mara moja kwa watu wazima wanaowatunga mimba wasichana wa umri mdogo katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Matiang’i amevitaka vyombo vya usalama kuanzisha uchunguzi na kuhakikisha kwamba wahusika wanatiwa mbaroni, akisema kaunti hiyo ndiyo iliyonakili visa vingi zaidi vya wasichana wa umri mdogo kutungwa mimba.

Waziri huyo amesema jumla ya wasichana elfu kumi wametungwa mimba katika kaunti hiyo.

Dkt. Matiang’i anazuru kaunti hiyo ili kukagua hali ya usalama na miradi ya maendeleo akiandamana na waziri mwenzake wa ugatuzi Eugene Wamalwa.

Waziri Matiang’i pia amepiga marufuku ‘disko matanga’ katika kaunti hiyo na akawaagiza machifu na manaibu wao kuhakikisha agizo hilo limezingatiwa.

Wasichana wengi wa shule walitungwa mimba wakati wa likizo ya miezi tisa ya mwaka uliopita iliyotokana na janga la korona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *