Mashua zote katika ziwa Naivasha kusajiliwa

Halmashauri ya shughuli za baharini KMA, imeanzisha mfumo mwafaka wa kusajili mashua zinazohudumu katika ziwa Naivasha katika juhudi za hivi punde za kukabiliana na ongezeko la visa vya uhalifu katika ziwa hilo.

Akiongea mjini Nakuru wakati wa mkutano wa pamoja baina ya wasimamizi wakuu wa halmashauri hiyo na maafisa wa serikali ya kaunti ya Nakuru wakiongozwa na gavana wa kaunti hiyo Lee Kinyanjui, mkurugenzi mkuu wa halmashauri hiyo Mutegi Njue alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto za usalama na kurejesha imani miongoni mwa wavuvi na wakazi wa eneo hilo.

Njue alitangaza kuwa halmashauri hiyo itaanzisha ngome ya kudhibiti usalama katika ziwa Naivasha ili kupiga jeki ngome ya doria ya vikosi vya kutoa ulinzi wa baharini.

Alisema kuwa ziwa Naivasha linakabiliwa na changamoto za kuzoa matope na mchanga na pia uchafuzi.

Alionya kuwa kundi lake halitasita kuwachukulia hatua kali wale wanaokiuka sheria za uvuvi na kutupa taka katika ziwa hilo.

“Mfumo uliowiainishwa wa utambuzi wa mashua utarahisisha halmashauri hiyo kuwatambua wavuvi haramu sawia na kuwapigia darubini wavuvi waliosajiliwa,” alisema Njue.

Gavana Lee Kinyanjui alisema kuwa serikali yake iko tayari kuipa halmashauri hiyo ardhi ya kujenga ngome ya kudumisha doria za usalama ambayo alisema itasaidia pia kuwapa mafunzo wahudumu wa mashua kuhusiana na mbinu za kuokoa maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *