Maseneta wa Marekani wapitisha mswada wa dola trilioni 1.9 za kukabiliana na athari za korona

Mswada wa Rais Joe Biden unaolenga kuwasaidia Wamarekani kukabiliana na athari za janga la COVID-19 umevuka kizingiti kikubwa baada ya kuidhinishwa na Bunge la Seneti nchini humo.

Mpango huo, wa dola za Marekani trilioni 1.9, uliidhinishwa na Bunge la Seneti Jumamosi licha ya kupingwa na maseneta wote wa chama pinzani cha Republican.

Baraza la wawakilishi ambalo lina wanachama wengi kutoka chama cha Rais Biden cha Democrat linatarajiwa kuidhinisha mswada huo Jumanne ijayo.

Biden alitaja hatua ya Bunge la Seneti kama hatua muhimu katika kutimiza ahadi yake ya kusaidia raia wa Marekani.

Hazina hiyo ambayo ni ya tatu tangu Marekani ianze kukabiliana na maradhi ya COVID-19 inahusisha utoaji wa malipo ya dola 1,400 kwa raia wengi wa nchi hiyo. Biden amesema malipo hayo yataanza kutolewa baadaye mwezi huu.

Janga la COVID -19 linakisiwa kuwa janga baya zaidi la Kiafya kuwahi kuikumba Marekani katika muda wa karne moja.

Janga hilo limesababisha takriban vifo vya watu elfu 523, huku wengine milioni 29 wakiwa wameambukizwa, nacho kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa asilimia 6.2.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *