Masaa ya kafyu kusalia kama yalivyo hadi mwisho wa mwezi Mei – Matiang’i

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Fred Matiang’i amesema amri ya kafyu iliyowekwa na Rais itaendelea kutekelezwa hadi tarehe 29 mwezi Mei, 2021.

Katika Kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Nakuru na Kajiado, kafyu hiyo ni ya kati ya saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri, huku kaunti zengine ikiwa ni kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Kwenye hotuba yake ya mwisho, Rais Uhuru Kenyatta hakubainisha muda wa utekelezaji wa agizo alilotoa kuhusu masaa ya kafyu, huku akisema lingetekelezwa hadi wakati ambapo agizo lengine litatolewa.

Lakini kupitia notisi ya Gazeti rasmi la serikali iliyochapishwa tarehe 12 mwezi Aprili, Matiang’i anasema agizo hilo litatekelezwa kwa muda wa siku 60 kuanzia tarehe 29 mwezi Machi, 2021.

Aidha, Matiang’i amejumuisha wadau wengine kwenye orodha ya wale ambao hawataathiriwa na agizo hilo, wakiwemo mawakili, watoaji huduma za kuwakinga watoto na wasimamizi wa sehemu za kuwanusuru wahasiriwa wa unajisi na maswala ya kijinsia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *