Marekani yatafuta mwafaka na China kuhusu utunzaji wa hewa

Mjumbe maalum wa Marekani John Kerry anaelekea huko Jijini Shanghai ili kuishawishi China kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusu hali ya hewa utakaoandaliwa na Rais Joe Biden juma lijalo.

Baada ya mzozo wa kidiplomasia kwenye Umoja wa Mataifa, pande zote mbili zilikubaliana kushirikiana katika juhudi za kupunguza uchafuzi wa anga.

Marekani inaitaka China kusitisha matumizi ya kawi inayotokana na mkaa wa mawe kwenye viwanda vyake vya kuzalisha umeme, na pia  kukoma kufadhili viwanda vya aina hiyo katika nchi za kigeni.

China inataka Marekani kutoa fedha zaidi kwa nchi zinazoendelea ili zijipatie teknolojia inayolinda mazingira na kuafikia viwango vya kimataifa vinavyokubalika vya utunzaji wa hewa.

Aidha, inaitaka Marekani nayo pia ipunguze shughuli za viwanda ili kupunguza uchafuzi wa hewa.

Wataalamu wa kisayansi wameonya kwamba bila makubaliano baina ya mataifa yanayoongoza katika uchafuzi wa hewa, hapana fursa ya  kuepusha janga kutokana na uchafuzi wa hewa duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *