Marekani yagomea uchaguzi mkuu wa Uganda

Marekani haitashiriki katika uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Alhamisi nchini Uganda.

Hii ni kutokana na hatua ya tume ya uchaguzi nchini humo kukataa asilimia 75 ya maombi ya Marekani ya kuwapa idhini waangalizi ili kushiriki katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani nchini Uganda Natalie Brown, tume hiyo haikutoa maelezo kuhusiana na uamuzi huo, licha ya kuwasilishwa kwa maombi kadhaa.

Amesema kuwa ni waangalizi wachache tu ndio walioteuliwa kutoka kwa kundi la watu 88.

Ameongeza kuwa uchaguzi huo mkuu wa Uganda utakosa uwazi na imani ambayo hutokana na kuwepo kwa waangalizi kutoka mataifa ya nje.

Raia wa Uganda watawachagua wabunge wapya na rais katika uchaguzi huo wa Alhamisi.

Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 35, atakuwa akiwania muhula wa sita mamlakani.

Hata hivyo Museveni anatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa upande wa upinzani Bobi Wine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *