Mamia ya raia wa Tunisia wakamatwa kufuatia maandamano dhidi ya kuzorota kwa uchumi

Polisi nchini Tunisia wamewatia nguvuni zaidi ya watu 600 huku usiku wa nne wa maandamano yenye ghasia ukishuhudia kurejea barabarani kwa waandamanaji hao.

Kwa mara nyingine siku ya Jumatatu, makundi ya waandamanaji vijana yalirejea kati kati ya mji mkuu, Tunis, huku wakiwashambulia polisi kwa mawe na mabomu ya petroli.

Maafisa wa usalama walijibu kwa kutumia vitoza machozi na pia mabomba ya maji.

Tunisia imeghubikwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, huku thuluthi moja ya vijana wa taifa hilo wakiwa hawana ajira.

Mgogoro huo wa kiuchumi umekuwa mbaya zaidi wakati huu wa janga la Corona.

Ghasia za hivi punde zinajiri miaka 10 baada ya mapinduzi yaliyoleta demokrasia nchini Tunisia na kuchochea maasi katika mataifa mbali mbali ya Kiarabu.

Hata hivyo, matumaini ya wengi eti hali hiyo ingewapa fursa nyingi za kikazi sasa yanazidi kudidimia.

Nje ya Jiji kuu la Tunis, ghasia ziliripotiwa Jumatatu katika miji mingine kama vile Kasserine, Gafsa, Sousse na Monastir.

Katibu wa Wizara ya Maswala ya Ndani alisema wengi wa wale waliotiwa nguvuni tangu kuzuka kwa ghasia siku ya Ijumaa ni vijana wenye umri mdogo ambao wamezuiliwa kwa kujihusisha na uporaji na uharibifu wa mali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *