Mamata Banerjee ashinda uchaguzi wa Jimbo la Bengal kwa mara ya tatu nchini India

Chama cha Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, kimeshindwa kupata jimbo muhimu kwenye uchaguzi ulioandaliwa huku kukiwa na ongezeko kubwa la vifo kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Chama hicho cha wazalendo wa Kihindu (BJP), kilitumia muda mwingi kwenye jimbo la Bengal Magharibi wakati wa kampeni, lakini eneo hilo limechukuliwa na mwakilishi wa sasa, Mamata Banerjee, ambaye ni mkosoaji mkuu wa Narendra Modi.

Chama hicho kilitamba katika Jimbo la Assam, lakini kikashindwa kupiga hatua muhimu kwingineko.

Shughuli ya kuhesabu kura ilifuatiliwa kwa makini ili kubaini iwapo Modi ataadhibiwa na wapiga kura kutokana na jinsi ambavyo ameshughulikia janga la COVID-19.

Kwa muda wa siku 10 mfululizo, maambukizi ya kila siku kutokana na janga la Corona nchini India yamekuwa zaidi ya watu elfu 300.

Siku ya Jumapili, India iliandikisha rekodi mpya duniani, baada ya kunakili vifo vya watu 3,689 kwa siku moja.

Hospitali za taifa hilo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa vitanda, na pia hewa ya oksijeni, huku raia wengi wakitumia mitandao ya kijamii kuitisha usaidizi.

Modi na waziri wake wa maswala ya nyumbani walihutubia mikutano kadhaa kwenye jimbo la Bengal Magharibi ambako walishtumiwa kwa kuelekeza jitihada zao kwenye uchaguzi badala ya janga la corona.

Baada ya kuhesabu karibu kura zote, chama cha Trinamool Congress party (TMC)chini ya uongozi wa Mamata Banerjee kimenyakua zaidi ya viti 200 kwenye bunge la viti 294.

Matokeo hayo yatamfanya Bi. Banerjee kuwa kiongozi wa Bengal Magahribi kwa mara ya tatu.

Aidha yeye ndiye mwanamke wa pekee anayeshikilia wadhifa wa waziri kiongozi nchini India.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *