Mamake Diamond afichua babake mzazi

Mama mzazi wa mwanamuziki tajika nchini Tanzania Diamond Platnumz ambaye anajulikana kama Bi. Sandra amefichua baba mzazi wa Diamond.

Bi Sandra, Sanura Kassim, ambaye anajiita Mama Dangote kwenye mitandao ya kijamii alitangaza haya kupitia kituo cha redio cha Wasafi Fm ambacho kinamilikiwa na mwanawe.

Mohamed Salum Iddy maarufu kama Ricardo Momo ambaye hufanya kazi kwa karibu na mwanamuziki Diamond alikuwa akihojiwa kituoni humo ambapo alifichua kwamba yeye na Diamond ni watoto wa baba mmoja.

Hapo ndipo mtangazaji wa kipindi cha mashamsham kwa jina Dida aliamua kumpigia simu mama Dangote ili kudhibitisha. Mama Dangote alithibitisha kwamba Diamond ni mtoto wa Marehemu Salum Iddy Nyange ambaye ndiye baba mzazi wa Ricardo Momo.

Kwa muda sasa Diamond amejikuta pabaya huku akilaumiwa kwa kumtelekeza babake ambaye wengi walidhani ni Mzee Abdul aliyekuwa mume wa Bi. Sandra lakini Sandra alielezea kwamba alimwoa akiwa tayari ana ujauzito wa Diamond.

Diamond amesutwa sana kuhusu kutelekeza babake kiasi cha kutungiwa wimbo na mwanamuziki Harmonize au ukipenda Konde Boy.

Alipohojiwa baada ya ufichuzi wa baba mzazi wa Diamond, Mzee Abdul alisema anafurahia maanake ni kama ambaye ametua mzigo mzito huku akimsihi Diamond aache kutumia jina lake “Abdul” na kwamba anamtakia kila la heri maishani.

Jina halisi la Diamond ni “Nasibu Abdul”.

Mzee Abdul alisema hakujua kuhusu uzazi halisi wa Diamond hadi alipofichua Bi Sandra hiyo jana.

Tangu jana Bi. Sandra amekuwa akiweka picha za zamani za Diamond na marehemu Salum Iddy Nyange na watumizi wa mitandao wanasema wawili hao wanafanana.

Kwa muda mrefu Ricardo Momo amekuwa akijitambulisha kama kakake Diamond na wengi hawakujua undugu wao hadi jana.

Ricardo alielezea kwamba Diamond alitambulishwa kwake rasmi mwaka 1999 na marehemu babake Salum Iddy Nyange, na wakati huo Diamond alikuwa na umri wa miaka 10.

Hii ina maana kwamba Queen Darleen na Diamond Platnumz hawana ukoo wa damu ila tu walilelewa na mzee Abdul.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *