Malkia Strikers yaendeleza mazoezi Kasarani kujiandaa kwa Olimpiki
Timu ya wanawake ya voliboli maarufu kama Malkia strikers imeendeleza mazoezi yake mapema Jumatano katika ukumbi wa Kasarani kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki watakapokuwa wakishiriki kwa mara ya tatu .
Vipusa hao ambao wamo kambini katika chuo kikuu cha Kenyatta watalenga kuandikisha historia , baada ya kukosa kunyakua hata seti moja katika makala ya mwaka 2004 mjini Athen Ugiriki wakishiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza na 2008 mjini Beijing China.
Hata hivyo wachezaji wengi wa timu ya taifa wangali na vilabu vyao kujiandaa kwa mashindano ya klabu bingwa Afrika nchini Tunisia baadae mwezi huu ambapo Kenya itawakilishwa na mabingwa wa ligi Prisons ,Kenya Commercial Bank na Kenya Pipeline walionyakua nishani ya shaba mwaka 2019.
Mashindano ya Afrika baina ya vilabu vya wanawake yataandaliwa mjini Souse Tunisia kati ya tarehe 16 na 28 mwezi huu.
Malkia Strikers pia wamepangiwa kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu nje ya nchi kujiandaa kwa mashindano ya Olimpiki wakiwakilisha bara Afrika.
Strikers wamejumuishwa kund H katika miechezo ya Olimpiki ya mwaka huu pamoja na mabingwa mara mbili wa Olimpiki Brazil,Jamhuri ya Dominika ,Korea Kusini na Serbia.