Mahindi kutoka Tanzania na Uganda yanapenyezwa humu nchini kutumia pikipiki

Kufuatia uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku uagizaji wa mahindi kutoka Uganda na Tanzania,wafanyibiashara katika kaunti ya Busia sasa wameamua kutumia mbinu mbadala za kuingiza bidha hiyo humu nchini.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la KNA ulidokeza kuwa wafanyibiashara kadha wameamua kutumia piki piki kusafirisha mahindi hayo hadi humu nchini.

Shirika hilo la habari lilibaini kuwa wahudumu wa boda boda wanasafirisha kati ya magunia mawili na matatu ya zao hilo kwa safari moja kupitia sehemu ya mpakani ya Sophia bila maafisa wa usalama kuchukua hatua zozote.

Magunia hayo ya mahindi yanahifadhiwa kwenye bohari moja kwenye kituo cha mabasi cha Busia kusubiri kusafirishwa kwa malori hadi sehemu mbali mbali nchini.

Alipohojiwa,afisa mkuu wa halmashauri ya kilimo na Chakula kwenye kaunti ya Busia Philemon Masinde alisisitiza kuwa uagizaji wa mahindi hayo kutoka nje siyo halali na wahusika wanapaswa kutiwa mbaroni mara moja.

Kwenye barua,tarehe tano mwezi huu iliyotiwa saini na kaumu mkurugenzi mkuu wa halmashauri hiyo ya kilimo na chakula Kello Harsama, serikali iliharamisha uagizaji wa mahindi kutoka Uganda na Tanzania baada ya vipimo kubaini kuwa yalikuwa na sumu ya aflatoxin.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *