Mahakama yazuia kuapishwa kwa Anne Kananu kuwa Kaimu Gavana wa Nairobi

Mahakama Kuu imetoa agizo la kuzuia kwa muda, shughuli ya kuapishwa kwa Anne Kananu Mwenda kuwa Kaimu Gavana wa Kaunti ya Nairobi.

Kwa mujibu wa agizo hilo, Kananu hataapishwa hadi kesi iliyowasilishwa na Chama cha Mawakili (LSK) na Tume ya Haki za Kibinadamu humu nchini (KHRC) itakaposikizwa na kuamuliwa.

Aidha, mahakama hiyo imemtaka Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kuteua jopo la majaji wasiopungua watatu, watakaotoa uamuzi kuhusu kesi hiyo.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya Kananu kukabidhiwa wadhifa huo na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura, ambaye alichukua hatamu hizo baada ya kubanduliwa mamlakani kwa aliyekuwa Gavana Mike Sonko.

Mutura alivaa kofia ya Kaimu Gavana kutokana na kutokuwepo kwa naibu gavana katika kaunti hiyo, hatua iliyoashiria kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo kauntini humo.

Hata hivyo, Anne Kananu, aliyeteuliwa na Sonko ili awe naibu wake tangu mwezi Januari mwaka uliopita, alisailiwa na kuidhinishwa Ijumaa iliyopita na Bunge la Kaunti ya Nairobi na hatimaye kuapishwa kuwa Naibu Gavana.

Kulingana na Mutura, kupatikana kwa naibu gavana wa kaunti hiyo kulimaanisha kwamba anafaa kuchukua wadhifa wa kaimu gavana kwa muda uliosalia hadi uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *