Mahakama ya Meru yasitisha huduma kutokana na maambukizi ya COVID-19

Huduma katika mahakama za Meru zimesitishwa kwa sababu ya msambao wa virusi vya Korona.

Kulingana na arifa iliyotolewa na Jaji Mkuu David Maraga, baadhi ya wafanyakazi katika mahakama hiyo, mawakili na wafanyakazi wao walithibitishwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo na kusababisha kufungwa kwa mahakama hiyo.

Agizo hilo litakaloanza kutekelezwa kesho litadumu kwa muda wa wiki mbili ili kutoa nafasi kuwekwa kwa mikakati ifaayo kuzuia msambao zaidi.

“Tumeamua kwamba shughuli na huduma zote za mahakama zinazohusu watu kutangamana katika Mahakama ya Meru zisimamishwe kwa siku 14 kuanzia Jumatatu tarehe 23 Novemba, 2020,” amesema Jaji Mkuu.

Hata hivyo, Maraga amekubali kesi za dharura kusikilizwa kupitia video.

Ameongeza kuwa shughuli zitarejelewa katika mahakama hiyo baada ya maafisa kupimwa na kuthibitishwa kwamba hawana virusi vya Korona na maafisa wa wizara ya afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *