Mahakama ya Kericho yafungwa kwa muda

Kaimu wa jaji mkuu Philomena Mwilu ameagiza kufungwa kwa muda kwa mahakama ya Kericho kutokana na ubovu wa jengo lake.

Kwenye taarifa Mwilu alisema shughuli za mahakama hiyo zitasitishwa kwa muda wa majuma mawili.

Muda huo utaruhusu jengo hilo kufanyiwa ukarabati ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wake.

Hatua hiyo imechukuliwa kuambatana na ripoti iliowasilishwa kwa idara ya mahakama iliyotaka jengo hilo likarabatiwe kwa dharura ili kuepusha kutokea janga.

Ripoti hiyo ilionyesha dosari za kimjengo kutokana na ukarabati uliofanyiwa jengo hilo mwaka wa 2014.

Ripoti hiyo ya uchunguzi iliwasilishwa kwa idara ya Mahakama tarehe 3 mwezi Machi mwaka 2021.

Msajili mkuu Anne Amadi alishuhudia kufungwa kwa jengo hilo na ndiye aliyeongoza kamati ya watumiaji wa mahakama kutathmini shughuli ya ukarabati wa jengo hilo na kuhamishwa kwa shughuli zake hadi jengo la kituo cha marekebisho ya tabia kwa muda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *