Magoha awataka wakuu wa shule kutorudisha wanafunzi nyumbani kwa ukosefu wa karo

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kwa mara nyengine ameagiza walimu wakuu wa shule za msingi na upili kuhakikisha wanafunzi wanaofika shuleni wanasajiliwa bila kujali karo wanazodaiwa.

Akiongea leo katika Shule ya Msingi ya Olympic Kaunti ya Nairobi, Magoha amesema agizo hilo linahusu shule za umma na za kibinafsi.

“Kwa mara nyengine, nawasihi wakuu wa shule kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayerudishwa nyumbani kwa sababu ya karo, katika shule za umma na za kibinafsi,” amesema Magoha.

Aidha, Magoha amesema masomo yataanzia mahali wanafunzi walipoachia na kwamba masomo ya kupitia mtandaoni hayatazingatiwa kama sehemu ya silabasi iliyoshughulikiwa.

Hali ya kufunga shule kwa muda mrefu imewaathiri vibaya wanafunzi hasa wasichana huku visa vya mimba na ndoa za mapema vikiripotiwa kuongezeka.

Akiwatahadharisha wahusika wa mimba za mapema kuwa watachukuliwa hatua ya kisheria, Waziri amewahimiza wasichana ambao wametungwa mimba baada ya shule kufungwa kwa muda mrefu kutokana na chamuko la ugonjwa wa COVID-19 kufika shuleni.

“Kwa wale wanafunzi wasichana ambao ni wajawazito, huku tukiwashughulikia wahalifu wa vitendo hivyo, nawahakikishia kuwa hakuna kitu cha kuogopa, warudi shule, walimu wawahurumie na wawasaidie. Wakati ukifika wapewe nafasi wakajifungue kisha warudi waendelee na masomo yao,” akaongeza.

Shule zilifungwa mnamo kati kati ya mwezi Machi kufuatia chamko la virusi vya corona humu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *