Magoha akosoa vyombo vya habari kwa kuangazia changamoto pekee katika ufunguzi wa shule

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amevishtumu vyombo vya habari kwa kuangazia zaidi upande wa changamoto kuliko mafanikio kwenye shughuli za kurejelewa kwa masomo humu nchini.

Magoha amesema serikali inashughulikia ipasavyo maslahi ya wanafunzi na kuvitaka vyombo vya habari kuangazia yaliyo mema katika sekta hiyo.

Waziri huyo amevikosoa vyombo vya habari akisema havitoi taarifa kuhusu ufanisi wa sekta hiyo na badala yake vinaangazia changamoto pekee.

Aidha, amevisuta vyombo vya habari kwa kutoa taarifa zisizofaa kumhusu badala ya kushirikiana na Wizara ya Elimu kuwapa moyo wanafunzi wakati huu mgumu ambapo taifa linakabiliana na janga la COVID-19.

Akiongea wakati wa hafla ya staftahi na waandhishi wa habari, Magoha amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwa kwenye mstari wa mbele kuiwezesha jamii kukabiliana na changamoto ibuka.

Amesema serikali inajizatiti kutatua tatizo la miundo mbinu finyu shuleni, akisema serikali imetenga shilingi bilioni 15 ili kuboresha mazingira ya shule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *