Magix Enga aungwa mkono

Mtayarishaji muziki nchini Kenya Magix Enga anaendelea kuungwa mkono baada yake kutangaza nia ya kuwania Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Mtangazaji wa redio Maina Kageni ndiye wa hivi punde kuonyesha hiari ya kuunga mkono Magix katika kuwania kiti cha Urais.

Akizungumza wakati wa mahojiano, Maina alisema atamuunga mkono Magix kwa kumpigia kura na atasaidia pia kwenye kampeni.

Maina Kageni alisifu kujitolea kwa Magix kwa kila anachokifanya akisema ni mtu ambaye huwa hafi moyo na ana matumaini.

Aliendelea kuomba vijana wote kuunga mkono Magix Enga wakati utakapowadia kwani ni mmoja wao kwa nia ya kuupa nafasi uongozi wa vijana.

Magix Enga hana uzoefu wowote katika siasa au uongozi lakini anajiamini sana na alitangaza nia ya kuwania urais kupitia mitandao ya kijamii.

Baadhi ya wafuasi hawaamini mambo haya na kulingana nao, Magix anajitafutia tu umaarufu wala hana haja na uongozi ila wanaomwamini walimsemea maneno ya kumtia moyo.

Sasa anaungana na watu wengine mashuhuri ambao wameonyesha nia ya kuwania nyadhifa za uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Mwanamuziki Prezzo ameshatangaza kwamba atawania kiti cha ubunge katika eneo bunge la Kibra kaunti ya Nairobi, VDJ Jones anamezea mate ugavana wa Kaunti ya Nairobi huku mwanahabari Jackie Maribe akionyesha nia ya kuingilia siasa ikiwa atapata hiyo nafasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *