Maggy Bushiri arejea Tanzania

Mwanamuziki Maggy Bushiri amerejea nchini Tanzania kutoka Marekani anakoishi kwa ajili ya kuzindua nyimbo kadhaa.

Alikuwa ameandamana na mpenzi wake kwa jina Martin Classic ambaye pia ni mwanamuziki na wameshirikiana katika nyimbo kadhaa. Wawili hao waliwasili wakiwa wamevalia barakoa nyeusi ila walizivua mara tu walipolakiwa na wenyeji wao.

Barakoa hazitumiki nchini Tanzania hasa baada ya serikali nchini humo kutangaza mwaka jana kwamba ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeisha humo.

Maggy Bushiri ni mzaliwa wa Congo, ila alilelewa nchini Tanzania kwa muda kidogo na baadaye yeye, ndugu zake na mamake wakahamia marekani kama wakimbizi.

Kulingana naye, aliondoka Tanzania akiwa na umri wa miaka miwili kuelekea Mozambique na baadaye wakaelea Marekani.

Alipohojiwa mwaka 2019 nchini Tanzania, alielezea kwamba babake aliaga dunia kabla wagure Tanzania na mamake akaaga dunia mwaka 2009 wakiwa nchini Marekani.

Kwenye mahojiano hayo pia alifichua kwamba alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Los Angeles anakoishi na anasomea mambo ya uanahabari hasa uundaji wa vipindi.

Mwaka 2018 alihojiwa na jarida la Los Angeles kwa jina “VoyageLA” ambapo alifichua kwamba haikuwa rahisi kuingilia muziki kwani mara nyingi aliambiwa hatoshi.

Wimbo wake ambao anasema ulifanya ajulikane zaidi ni “Swing Your Body”. Wakati huo alifichua mipango yake ya siku za halafu, ile ya kufungua kampuni ya mavazi ambapo rangi kuu itakuwa Zambarau au ukipenda Purple.

Anapenda sana rangi hiyo naye hujiita “The Purple Queen” ila alipowasili Tanzania jana, hakuwa na nywele za rangi ya Zambarau kama siku za awali.

Alizungumzia pia mipango ya kurejea alikozaliwa na kuanzisha kituo kikubwa ambacho kitakuwa makazi ya kuhudumia mayatima.

Inasubiriwa sasa kuona mazuri ambayo ameletea mashabiki wake wa Tanzania mwaka huu wa 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *