Magavana waapa kuwapiga kalamu wahudumu wa afya wanaogoma

Magavana wametishia kuwaachisha kazi wahudumu wote wa afya wanaogoma iwapo hawatarejea kazini mara moja.

Magavana hao pia wamefichua kwamba watasambaza majina ya wafanyanyikazi wote watakaofutwa kazi kufuatia mgomo huo katika kaunti zote ili wasiajiriwe tena kwenye kaunti zengine.

Kwenye kikao na wahariri wa habari, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya ameutaja mgomo huo kuwa kinyume cha sheria.

“Tumesikitishwa na uamuzi wa muungano wa wahudumu wa afya kutekeleza mgomo ambao umedumu kwa mwezi mmoja licha ya janga [la COVID-19] na maagizo ya mahakama. Tunaichukulia hatua hii kuwa kinyume cha haki ya maisha na ya kupata viwango vya juu zaidi vya huduma ya afya kama inavyohakikishwa katika katiba,” akasema Oparanya.

Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega, amesema wahudumu hao walipaswa kutamatisha mgomo wao ili kusubiri matokeo ya mashauriano kati ya Wizara ya Leba na ile ya Afya.

Gavana huyo amesema swala la nyongeza ya mishahara kama wanavyodai wahudumu hao ni jukumu la Tume ya kuratibu mishahara ya watumish wa umma, SRC na Wizara ya Fedha nchini.

Oparanya ameongeza kuwa serikali za kaunti zimejitolea kuhakikisha maslahi ya wahudumu wa afya yameshughulikiwa lakini akatahadharisha kuhusu matakwa mengi ya wahudumu hao kwani uchumi wa nchi hii umeathiriwa pakubwa na janga la COVID-19.

Baadhi ya serikali za kaunti, ikiwemo ile ya Mombasa, tayari zimechukua hatua ya kuwaachisha kazi wahudumu wa afya wanaogoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *