Madereva wa malori wataka muda wa matumizi ya vyeti vya Corona uongezwe

Madereva wa malori ya safari ndefu wanaomba Wizara ya Afya kufanyia marekebisho masharti ya kupimwa virusi vya Corona kila baada ya siku 14.

Madereva hao wanadai kwamba hitaji hilo haliwezi kutekelezwa kwani inawachukua siku hizo 14 kusafiri kutoka bandari ya Mombasa kwenda maeneo kadhaa ya kanda ya Afrika Mashariki.

Madereva waliozungumza katika mji wa mpakani wa Malaba ulioko Kaunti ya Busia wanasema kipindi hicho cha wiki mbili kinawagharimu zaidi kwani wengi wao hutumia hata zaidi ya siku 14 kusafiri kati ya Mombasa na mataifa mengine ya kanda hii.

Mmoja wa madereva hao, Alex Wambua, amesema vyeti vyao vya kuthibitisha hali yao ya kiafya hufikia muda wa mwisho kabla ya kurejea nchini kwa hivyo wanalazimika kutumia kiasi cha shilingi 7,000 za Kenya ili kupimwa virusi hivyo nchini Sudan Kusini na Uganda.

“Wiki mbili ni muda mfupi sana. Tunaomba serikali ya Kenya ilete mfumo ambapo madereva wanapimwa kila baada ya siku 30 badala ya siku 14 kwa sababu baadhi yetu tunatumia muda huo wa siku 14 kusafiri hadi Kampala, Kigali au Juba,” akasema Wambua.

Dereva mwingine, Seneta Mwashumba, ambaye alikuwa akielekea Juba, anasema msongamano wa magari katika mji huo wa mpakani bado ni shida hata baada ya kuanzishwa mfumo wa madereva kupimwa kabla ya kuanza safari.

Mwashumba anadai kwamba wanazuiiwa kwenye mpaka wa Malaba kwa siku tatu zaidi.

“Kwa mfano mimi tayari nimepimwa, niko na cheti na lori langu limeidhinishwa kusafiri. Lakini sijaweza kuanza safari na nimekwama hapa kwa siku tatu,” akasema.

Madereva wengine wanasemekana kutumia siku 11 kati ya Mombasa na Bungoma kabla ya kujiunga na foleni mpakani ambapo wanapaswa kutumia siku nyingine nne na kulazimika kupimwa tena baada ya kukamilika kwa siku 14.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *