Madaktari waahirisha kuanza kwa mgomo wao hadi tarehe 21 Desemba

Chama cha Kitaifa cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU) kimefutilia mbali mgomo uliopangiwa kuanza leo.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Chibanzi Mwachonda amesema Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa chama hicho lilikutana na kuamua kutoa ilani mpya ya siku 14 ya mgomo ili kutoa fursa ya mashauriano kuhusu matakwa yao.

Chama hicho kinasema ikiwa maswala ambayo wameibua hayatashughulikiwa katika muda huo wa siku 14, basi mgomo huo utaanza tarehe 21 Desemba.

Katika taarifa kwa wanachama, Mwachonda amewahimiza Madaktari kutohatarisha maisha yao popote ambako hakuna vifaa vya kujikinga hasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Uamuzi wa kusimamisha mgomo huo umeafikiwa baada ya mabunge yote mawili kuonyesha kwamba kamati zao za afya zinapanga kukutana tarehe 9 na 10 Desemba kujaribu kusuluhisha masuala yaliyozua utata.

Miongoni mwa masuala yanayozozaniwa ni pamoja na kuwapa vifaa vya kutosha vya kujikinga, maafisa wote walioorodheshwa miongoni mwa makundi ya walio hatarini kutojumuishwa katika majukumu ya mstari wa mbele, kuwepo mpango makhsusi wa bima ya matibabu, kupandishwa vyeo, kuorodheshwa kulingana na majukumu yao na kuwianishwa kwa marupurupu yao ya kufanya kazi katika mazingira hatari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *