Madaktari kuanza mgomo wao Jumatatu huku wauguzi nao wakidinda kurejea kazini

Chama cha Kitaifa cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU) kimetangaza kuwa madaktari wote watagoma kuanzia Jumatatu baada ya mashauri na serikali kugonga mwamba.

Kwenye taarifa ya umma, chama cha KMPDU kimesema hatua hiyo inatokana na masuala ambayo hayajasuluhishwa baada ya mashauriano ya miezi minane.

“Madaktari watasitisha huduma zao kutokana na masuala ambayo hayajasuluhishwa baada ya miezi minane ya mashauriano kati ya KMPDU na serikali,” imesema taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo, makundi ya madaktari watakaogoma kuanzia tarehe 21 mwezi huu ni wanagenzi wa matabibu, wanagenzi wa taaluma ya dawa, wanagenzi wa taaluma ya wataalamu wa meno na matabibu.

Wengine ni wataalamu wa dawa, wataalamu wa matibabu ya meno, wataalamu wa utoaji huduma maalum za matibabu na wasimamizi wote wa maafisa wa huduma za utabibu.

Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwaonya wahudumu wa afya wanaogoma kurejea kazini la sivyo wafutwe kazi.

Wauguzi na matabibu wamekuwa wakigoma tangu Jumatatu juma lililopita, wakishinikiza bima bora ya afya na kupewa vifaa vya kujikinga wanapokuwa kazini, miongoni mwa masuala mengine.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako amepuuzilia mbali agizo la Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwa warejee kazini.

Panyako alikuwa akiongea huko Kakamega wakati wa mazishi ya Wycliffe Alumasa, ambaye ni muuguzi aliyepoteza maisha yake kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Alisema hakuna agizo lolote la mahakama ambalo litawalazimisha kurejea kazini kuambatana na mazingira yaliyoko sasa, ambapo hakuna vifaa vya kujikinga wala mpango wa bima ya matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *