Machifu watakiwa kuhakikisha wanafunzi wote wamerejea shuleni

Kamishna wa kaunti ya Narok Evans Achoki amewaagiza machifu wote na manaibu wao katika kaunti hiyo kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni katika maeneo yao ya kazi.

Akiongea wakati wa mkutano wa hadhara katika sehemu ya Okurto kaunti ndogo ya Narok Kaskazini, Achoki amesema ni sera ya serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni.

Alisema takriban asilimia  94 ya wanafunzi katika shule za msingi za umma na asilimia 98 ya wanafunzi wa shule za upili za umma katika kaunti ya Narok wamerejea shuleni.

Amesisitiza kuwa hata kama wanafunzi hao walioa ua kuolewa au kutungwa mimba au kujihusisha katika aina yoyote ya ajira ya watoto ni sharti wapatiwe fursa ya kukamilisha masomo yao.

Achoki amewatahadharisha wazazi dhidi ya kuhusisha watoto wao katika tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji wa wasichana na ndoa za mapema.

Kamishna huyo amesema mtu yeyote atakayepatikana akiendeleza tamaduni hizo atakabiliwa kisheria.

Watu kadhaa katika kaunti hiyo wameshtakiwa Mahakamani kwa kukeketa wasichana wadogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *